shuku image TIA MBEYA

Friday, May 4, 2012

Msichana aongoza mtihani kidato cha sita

  Ni wa Sekondari ya Marian Girls
  Ufaulu waongezeka mwaka huu
  Shule za serikali zafanya vizuri
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako
Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka huu huku msichana Faith Assenga, wa Shule ya Sekondari Marian Girls, iliyoko Bagamoyo mkoani Pwani, akiongoza kwa wanafunzi watano bora kitaifa.

Aidha, watahiniwa 3,404 sawa na asilimia 7.73 waliofanya mtihani huo, wamefeli kwa kupata daraja la sifuri huku wanafunzi 5,635 sawa na asilimia 12.80, wakiambulia daraja la nne ambalo pia haliwezi kuwasaidia kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, alisema ufaulu wa mtihani huo kwa mwaka huu umeongozeka kwa asilimia ndogo huku pia idadi ya wanaofanya udanganyifu ikipungua.

Alisema watahiniwa waliofanya mtihani huo walikuwa 44,190 ambapo asilimia 5.67 ambao ni 2,499 ndio waliopata daraja la kwanza, wakati waliofaulu kwa daraja la pili ni 9,126 sawa na asilimia 20.72. Alisema waliopata daraja la tatu ni 23,375 sawa na asilimia 53.08.

Hata hivyo, Dk. Ndalichako, alisema jumla ya watahiniwa 46,499 sawa na asilimia 87.58 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la nne ikilinganishwa na watahiniwa 49,653 sawa na asilimia 87.24 ya waliofaulu mwaka jana.

Alisema wavulana 30,466 sawa na asilimia 87.69 wamefaulu mtihani huo wakati wasichana 16,033 sawa na asilimia 87.37 ndio waliofaulu.

Kwa mujibu wa Dk. Ndalichako, watahiniwa wa shule wamefanya vizuri zaidi kuliko wale wa kujitegemea ambapo waliofaulu ni 40,635 sawa na asilimia 92.27 wakati watahiniwa 5,864 sawa na asilimia 64.75 wa kujitegemea wamefaulu.

Kuhusu waliofeli, Dk. Ndalichako alisema wavulana 2,229 wamepata daraja sifuri ikilinganishwa na wasichana 1,175 huku wavulana 3,659 wakipata daraja la nne na wasichana 1,976 wakipata daraja hilo.

Kadhalika, sekondari za serikali zimefanya vizuri kwenye matokeo hayo ambapo shule sita za umma zenye watahiniwa 30 na zaidi zimeingia kwenye shule 10 bora kitaifa wakati za binafsi zikiwa ni nne kwenye kundi hilo.

Aidha, Dk. Ndalichako alisema ufaulu umeongezeka kwa masomo ya lugha, biashara, Historia, Jiografia, Fizikia, Hesabu na Bayolojia huku ufaulu wa masomo ya uchumi, Kemia na General Studies ukiwa umeshuka.

SHULE 10 BORA


Dk. Ndalichako alisema  Marian Girls ya mkoani Pwani imekuwa ya kwanza kwa shule 10 bora zenye watahiniwa 30 na zaidi ikifuatiwa na Feza Boys ya Dar es Salaam. Shule nyingine katika kundi hilo ikianzia ya tatu ni Kisimiri (Arusha), Kibaha (Pwani), Ilboru (Arusha), Mzumbe (Morogoro), Msalato (Dodoma), Tabora Boys (Tabora), St. Mary's Mazinde Juu (Tanga) na Seminari ya Consolata (Iringa).

Katika kundi la pili, Uru Seminari ya Kilimanjaro imeongoza shule zenye watahiniwa pungufu ya 30 ikifuatiwa na Iwawa (Iringa) na ya tatu ni Maua Seminari (Kilimanjaro).

Shule nyingine katika kundi hilo ni Harrison Uwata (Mbeya), Beroya (Ruvuma), Palloti (Singida), Lutengano (Mbeya), Makita (Ruvuma), Mwanga (Kilimanjaro) na Visitation Girls (Kilimanjaro).

"Shule 10 za mwisho kitaifa katika kundi la shule zenye watahiniwa 30 na zaidi ni Pemba Islamic College ya Pemba ikifuatiwa na Zanzibar Commercial ya Unguja," alisema.

Alisema nyingine ni Kongwa (Dodoma), Uweleni (Pemba), Mazizini (Unguja), Lumumba (Unguja), Ben Bella (Dodoma), Mlima Mbeya (Mbeya), Laureate International (Unguja) na Haile Selassie (Unguja).

Katika mtiririko huo, Dk. Ndalichako alizitaja shule 10 za mwisho zenye watahiniwa pungufu ya 30 ni Mbarali Preparatory (Unguja), Philter Federal International (Unguja), High View International (Unguja), Kifai Modern (Dar), Sha (Unguja), Dar es Salaam Prime (Dar), Kandoto Sayansi (Kilimanjaro), Popatlal (Tanga), Al-Falaah Muslim (Unguja) na Kiuma (Ruvuma).

WANAFUNZI BORA KITAIFA

Akizungumzia wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kitaifa, Dk. Ndalichako alisema Necta imewapanga kulingana na ufaulu wa kombi zao 'combination' kuanzia sayansi, biashara na lugha na sayansi ya jamii.

Aliwataja waliofanya vizuri zaidi kwa masomo ya sayansi kuwa ni Faith Assenga (PCM-Marian Girls), Zawadi Mdoe (PCM-Feza Boys), Belnadino Mgimba (PCM-Minaki), Jamal Juma (PCM-Feza Boys) na Imaculate Mosha (PCM-Marian Girls).

Alisema katika kundi la sayansi, wasichana bora watano kitaifa wametoka Marian Girls wakati sekondari ya wasichana Weruweru ikitoa wasichana wanne bora kitaifa wa masomo ya biashara kati ya watano.

Wakati huo huo, Necta imefuta matokeo ya watahiniwa sita waliobainika kufanya udanganyifu na wamezuiwa kufanya mtihani wa baraza hilo kwa mwaka mmoja.

Alisema watahiniwa hao walikutwa na majibu (notisi) kwenye chumba cha mtihani na kuonya kwamba baraza hilo litaendelea kuchukua hatua kali zaidi kwa watakaobainika kufanya vitendo hivyo pamoja na maofisa watakaohusika kusaidia kufanyika kwa uhalifu huo.

Aliongeza pia kuwa baraza hilo limezuia matokeo ya watahiniwa 51 ambao hawakuwa wamelipa ada ya mtihani huku likizuia matokeo ya watahiniwa 103 ambao hawakuwa na alama za maendeleo ya kila siku.

Alisema matokeo yaliyozuiliwa yatatolewa baada ya wahusika kukamilisha kulipa ada hiyo pamoja na faini na baada ya wakuu wa shule kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya kila siku ya mwanafunzi.

No comments:

Post a Comment