shuku image TIA MBEYA

Tuesday, March 5, 2013

Jinsi ya kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio.


Mtu yeyote anapoingia katika maisha huwa anakabiliwa na changamoto ya kuamua kati ya kujiajiri au kuajiriwa. Kuajiriwa kunakuhakikishia usalama kazini japokuwa usalama huo siku hizi ni nadra sana kuwepo, wakati kujiajiri hukuhakimkishia uhuru wa kuamua mambo yako. Watu wengi huamua kuchagua kuajiriwa kwa sababu ni rahisi kuliko kuwa wajasiriamali ambako ni kugumu, tatizo wanalolipata ni kuwa wanaishi kwa kutegemea mshahara ambao huwa hautoshi na kujiingiza kwenye madeni mabaya ambapo hukopa kwa ajili ya matumizi na kuendelea kuwa na madeni makubwa zaidi. Kukopa siyo kubaya ila kuna madeni mabaya na madeni mazuri madeni mabaya ni yale ambayo mtu anakopa kwa ajili ya hela ya kula au kutumia, madeni mazuri ni yale ambayo mtu anakopa kwa ajili ya kuwekeza kwenye vitegauchumi au kwenye biashara kwa kufanya hivyo mtu anaweza kujitoa kwenye matatizo.

Wengine wanapata mishahara mikubwa lakini wanashindwa kutumia pesa zao vizuri kwa kujiingiza kwenye maisha ya anasa na kuwa kwenye madeni makubwa. Kwa mfano unaweza kukuta mtu amenunua magari manne ya kutembelea wakati ambapo angeweza kuwa na gari moja na akawekeza kwenye kujenga nyumba za kupangisha na kuweza kujiingizia kipato. Uamuzi wa kuajiriwa ni sawa na kuwa kifungoni hupaswi kuishi katika hali hii unahitaji kuwa huru. Njia ya kujinasua katika tatizo hili fanya yafuatayo; wakati uko kazini ukiwa umeajiriwa unaweza kuanza kufanya juhudi za kujikwamua kwa kuanzisha miradi midogo midogo au kujishughulisha na kuwekeza kwenye vitegauchumi pesa zako ili ziweze kukusaidia baadaye.
Uamuzi wa kujiajiri na kuwa mjasiriamali unakusaidia kuwa huru, kupata kila kitu ukitakacho, kufanya kitu ukitakacho, kufikia malengo yoyote uliyojiwekea. Unaweza kubadilisha maisha yako unachopaswa kufanya ni kujiamini kumbuka kwamba njia hii ya kuelekea kwenye mafanikio siyo rahisi ndiyo maana njia hii huwa inachaguliwa na wachache kiasi kwamba asilimia 90% ya utajiri wa dunia unashikiliwa na asilimia 10% ya wajasiriamali. Kitu kinachowakwamisha watu wengi ni kuwa na hofu ya kufilisika endapo mtu atawekeza na kufilisika. Ufumbuzi wa tatizo hili ni ni kuwa na ufahamu kwa kupata elimu ya ujasisriamali. Hivyo ndivyo dunia ilivyo, dunia inabadilika hivyo inabidi na sisi tubadilike.

Nimekuwa nikifuatilia maisha ya wastaafu jinsi wanavyopata taabu kwa kutegemea pensheni ambazo hazitoshi,wengine wamekuwa wakirudi kazini kutafuta kazi za mikataba hali ambayo ingeepukwa kama angekuwa na maarifa tunayofundisha hapa. Kwa hiyo ili uepuke maisha ya kuadhirika uzeeni unapaswa kuanza kujiandaa sasa hivi. Sikushauri kwamba uache kazi sasa hivi unaweza kuanza kidogo kidogo, kwa mfano unaweza kuanza kutafuta eneo la kujenga makazi yako ya kudumu tafuta kuanzia ekari 1. Baada ya kujenga eneo lako unaweza kuanzisha biashara ndogo ndogo au kubwa kuanzia hapo nyumbani kwako zikiendeshwa na familia yako. Kwa mfano unaweza kufuga kuku wa kienyeji au wa kisasa, unaweza kufungua duka la reja reja au la jumla unaweza kuanzisha bustani, kuuza ice cream, maji nk. Biashara hizi zinaonekana ni ndogo lakini zinaweza kukuinua kiuchumi. Mapato yakiongezeka unaweza kutafuta viwanja vingine na kujenga nyumba za kupangisha vikiwa ni vitegauchumi ambavyo vinaweza kukusaidia katika wakati wa shida. Si vyema kuacha kazi kwenda kuendesha biashara hadi hapo unapoona biashara yako inakupatia kipato kingi kuliko kazi yako. Kipimo cha kujua kama unapata mapato mengi ni uwezo wa mapato ya biashara yako kugharimia matumizi yako kati ya miezi 6 hadi miezi 24 na mapato yako yawe mara 3 ya matumizi yako hapo ndipo unaweza kuacha kazi vinginevyo usiache kazi.
Anza kuwa na malengo ya juu ya maisha yako ukifikiria jee yatakuwaje miaka 5 ,10, 20 ijayo. Watu wengi huwa hawafikirii maisha ya baadaye na kitu hiki si cha mchezo kwani kama hukujipanga maisha yako yanaweza kuja kuwa magumu hasa uzeeni. Achana na kufikiria kuhusu kustarehe anza kutumia muda wako kupanga mipango na kuitekeleza mipango yako. Ukifikiria sana kuhusu mipango na malengo yako mwishoni utafanikiwa kimaisha na kiuchumi. Kama unataka kupata pesa nyingi zaidi fikiria jinsi ya kupata hizo pesa usifikirie kuhusu matatizo ya kukosekana pesa. Pia unapaswa kujua ni kiasi gani hasa cha pesa unachokihitaji. Weka malengo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kuwa unahitaji pesa kiasi gani. Lenga kufika mbali usifikirie malengo madogo madogo, katika mafunzo yangu huwa na waambia hakuna ubaya wa kujiwekea malengo ya kuwa tajiri na kuwa na mamilioni ndani ya benki na raslimali nyingi.

Watu wengi huwa na malengo ya kuwa matajiri bila kuwa na mikakati na mchakato wa kufikia malengo yao. Hata wakiwa na mikakati na mchakato wa kufikia malengo hushindwa kutekeleza kwa vitendo na kubaki na ndoto za alinacha. Watu wengi wanapenda kucheza bahati nasibu na kucheza kamari na hufikiria pesa zinadondoka kama mvua lakini hujikuta wakipoteza fedha na kuwa masikini zaidi. Ukitaka uwe masikini jiingize katika kucheza bahati nasibu na kucheza kamari . Ukianza kucheza kamari ujue unaukaribisha umasikini. Hakuna njia rahisi au ya mkato ya kufikia mafanikio. Unachotakiwa kufanya ni kuwa na malengo na kuchukua hatua kidogo kidogo kuelekea kwenye mafanikio. Hali hii inafanana na mtu ambaye anataka kujenga misuli kwa kufanya mazoezi kwa siku moja hata akijitahidi vipi haitawezekana sana sana ataishia kujiumiza au kujiua kama akijilazimisha. Maisha ni sawa na mkulima, mkulima huwa anapanda mbegu anasubiri iote, anapalilia, anaweka mbolea kisha ndipo anavuna mambo yote haya yanafanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja. Huwezi kupanda mbegu leo na ukategemea iote na uvune kesho yake hiyo ni akili ya kitoto, ukiwa mtu mzima unahitaji kuwa na subira. Kama hujaanza kufikiria kuwa na biashara ya kufanya anza kufikiria sasa na kama unayo biashara unayoifanya sasa jiulize ni jinsi gani utakavyoiboresha jiwekee malengo ya kipindi cha miaka 5 kuanza kuona mabadiliko.

Mafanikio pia huwajia watu ambao wanalenga mbali ambao ni wavumilivu na wanaweza kusubiri kuanzia miaka 5 hadi 10 ili kuona mabadiliko, lakini ukiwa mtu mwenye haraka na maisha kila mara utakuwa unaanzisha kitu kisha unaacha na hutakamilisha chochote. Katika kitabu cha Napoleon Hill Think and grow rich kuna hadithi ya mtu mmoja asiye na subira alikuwa na mgodi akitafuta dhahabu, alichimba kwa miaka kadhaa bila kupata dhahabu, baadaye akawa amekata tamaa na kuondoka zake, kuna mtu mwingine aliingia kwenye shimo alilokuwa amechima baada ya kuchimba kina cha futi moja aliikuta dhahabu. Msomaji naomba usiwe mtu wa kukata tamaa, kila mtu ana biashara kubwa ndani yake kutokana na kipaji alichopewa na Mungu, lenga kutatua matatizo ya jamii inayokuzunguka utashangaa jinsi mawazo ya kupata pesa yatakavyoanza kukujia.



Charles ni mshauri wa biashara na Mtunzi wa kitabu cha mbinu za biashara
Kwa ushauri tembelea blogu yangu http://www.squidoo.com/mshauricharles

No comments:

Post a Comment