shuku image TIA MBEYA

Wednesday, May 16, 2012

Biashara ya kununua/kuuza nje ya nchi (import-export)

Wapendwa wasomaji nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati wasomaji wote walionipa mrejesho (feedback) katika mada ya wiki iliyopita tulipogusia kidogo juu ya kupanua biashara nje ya nchi.
Zaidi ya wasomaji 245 wameomba mada hii niiweke kwa upana zaidi. Nami sina ajizi kwani inanipa moyo kuwa kuna wajasiriamali wengi wanalenga kupanua biashara zao nje ya mipaka ya Tanzania ambapo itawaingizia faida zaidi na hata kwa upande wa nchi itaongeza pato la taifa (GDP) na kuinua uwiano wa bidhaa zinazoletwa nchini na zile zinazouzwa nje ya nchi (balance of payment- katika dhana ya kawaida).
Hivyo basi kuweka mada hii katika mapana yake  tutakuwa na mfululizo (series) wa mada kwa wiki 5 itakayohusu mambo ya msingi katika biashara ya kununua/kuuza nje ya nchi, kutengeneza mahusiano kibiashara, mchanganuo wa soko, wapi utapata msaada, namna ya kukutana na jamii ya wajasiriamali wanaojihusisha na biashara za kimataifa, upatikanaji na uuzaji wa bidhaa, makubaliano ya kibiashara, kufanya mauzo, taratibu za kusafirisha bidhaa (terms of shipping), utumiaji wa mawakala wa usafirishaji (freight forwarder), barua ya udhamini ( letter of credit), upokeaji bidhaa, namna ya kutangaza bidhaa nje, kupanua biashara na kukuza/kustawisha biashara ya kununua/kuuza nje. Nakusihi usikose  kupata nakala ya gazeti lako pendwa kila wiki ili kupata mfululizo wa mada hii adhimu.
Ni njia gani za kuanzisha biashara yenye mafanikio na unayoweza kuipenda? Biashara ya kununua/kuuza (import/export) nje ya nchi inaweza kuwa jibu lako. Si kwamba inahitaji tu mtaji mdogo kuanza bali pia inakupa fursa ya kukutana na wateja mbalimbali ulimwenguni kote. Hauhitaji uzoefu mkubwa kufanya biashara hii, japo unahitaji uwezo mzuri wa kuratibu na kusimamia mambo. Kufanya biashara hii istawi kunahitaji taarifa na umakini wa mambo muhimu sana.
Je wewe unazalisha bidhaa na ungependa kupanua soko nje ya nchi? Au je una mpango wowote wa kusafiri nje ya nchi ili kupata taarifa kwa ajili ya kuanzisha biashara? Kama una uwezo wa kushawishi wateja na uwezo wa kufanya mahusiano ya kimataifa, biashara ya kununua/kuuza nje ya nchi inaweza kuwa nzuri kwako. Unachohitaji ni ari na malengo ya kufanikiwa.
Kadili utakavyoendelea kufanya biashara, utaelewa mambo mengi na namna ya kutatua changamoto. Mathalani unaweza kuhitaji mtu wa kusimamia masuala ya usafirishaji (freight forwarder). Na ungependa kuwa na mawasiliano na uhusiano mzuri na wagavi (suppliers). Lakini baada ya muda fulani unaweza kufanya mwenyewe taratibu hizo kwa gharama nafuu.
Faida nyingine ya kununua/kuuza nje ya nchi ni uzoefu wa kimataifa na faida halisi kutokana na biashara. Mara unapokuwa umezoea biashara, gharama ya kufanya mauzo inakuwa ndogo sana.
Na baada ya kuwa umejiimarisha na kuwa na wateja wa kutosha, utaona muda wako wote unaingiza pesa tu. Ichanganue biashara ya kununua/kuuza nje ya nchi, angalia vihatarishi (risks), na pima faida. Ongea na watu mbalimbali wafanyao biashara kama yako ili kujipima.

INAWEZEKANAJE
Kwa mujibu wa takwimu za Word Bank (Doing business in Tanzania - 2011) uzalishaji unaofanyika Tanzania ni 0.2% tu ndio inauzwa nje ya nchi. Kimsingi bidhaa ambazo huuzwa nje ni zile zitokanazo na kilimo na mapambo.
Ni dhahili kila mzalishaji wa bidhaa angependa kupanua soko lake hadi nje ya nchi, lakini si rahisi sana kwa kampuni au biashara yenye upeo na uwezo mdogo.
Si ajabu nawe msomaji ukawa katika kundi hili. Cha kufanya unaweza kutafuta mawakala nje ya nchi kwa ajili ya kusambaza bidhaa zako.
Changamoto iliyopo kwa wazalishaji wengi Tanzania hakuna ubunifu wa kutosha na ari ya kujituma kuzingatia ubora na viwango vya bidhaa wanazozalisha. Hivyo ni msingi kutafuta mawakala au watu wanaoweza kukupatia maelekezo mazuri ya vigezo na namna utakavyouza bidhaa zako nchi za nje.
NAMNA YA KUANZA  
Biashara hii ya kuuza/kununua nje pia unaweza kuanzia nyumbani kwako kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii mfano facebook, twiter, email, n.k. unachohitaji ni mfumo mzuri wa kutunza taarifa, kuwa na business card, kuwa na komputa pamoja na simu aidha ya mezani au ya mkononi inayopatikana endapo mteja atahitaji kuwasiliana kwa njia hii.
Baada ya biashara kusimama utahitaji kujiimarisha zaidi kimawasiliano. Pia utahitaji kuwa na nembo na anuani ya biashara (letter head), kibiashara nembo ndiyo inakuwakilisha hivyo ni muhimu sana iwekwe kitaalam. Itaendele…………..+255753686848

1 comment:

  1. Nimefurahishwa na mada hii kwani nimekuwa na shahuku kubwa ya kufahamu namna ya kuuza bidhaa nje. Nitafufuatilia muendelezo wa madaa hii

    ReplyDelete