shuku image TIA MBEYA

Thursday, May 10, 2012

Jk atosa DC 51, aibua 70 wapya

10th May 2012
Chapa
Maoni
  Wamo wabunge na waandishi kibao
  Watapigwa msasa na kupewa mtihani
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Rais Jakaya Kikwete ameteua wakuu wa wilaya huku akiwaacha 51 wa zamani na kuteua wapya 70.

Miongoni mwa walioteuliwa, vijana wenye umri kati ya 35 hadi 40 ni 40, wanawake 43 wakiwamo wabunge wa Viti Maalum watano, huku waandishi wa habari watano wakiteuliwa kushika wadhifa huo.

Akitangaza wakuu hao wa wilaya jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema uteuzi wa vijana umezingatia pia kuwajengea uwezo kama viongozi wa baadaye.

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na mawaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Hawa Ghasia (Tamisemi), William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge), Naibu Mawaziri, Kassim Majaliwa (Elimu) na Aggrey Mwanri (Tamisemi), Pinda alisema wakuu wa wilaya 51 walioachwa ni kwa sababu mbalimbali, ikiwamo umri, maradhi na utendaji.

Pinda alisema mchakato huo umechukua muda mrefu kwa sababu ya kuongezeka kwa wilaya mpya 19 kutoka 114 hadi 133; hivyo ilichukua muda kuwachambua na kuwapanga.

“Tumetoa wiki moja, wakuu hawa wajiandae kwenda kwenye vituo vyao vya kazi, watatakiwa kuapa mbele ya mkuu wa mkoa halafu tutawapatia mafunzo kwa wiki mbili pale Dodoma tena nimewaambia watu wa Tamisemi wawape mtihani kabisa,” alisema.

Alisema mafunzo hayo yatawahusisha pia wakuu wote wa mikoa na makatibu tawala wote.

Alisema: “Sitaki iitwe semina. Ndio maana nimesema wapewe mitihani. Tunataka wakuu wa mikoa na wilaya watekeleze majukumu yao ipasavyo.”

MATUMIZI YA  FEDHA ZA UMMA

Akizungumzia matumizi ya halmashauri, Pinda alisema serikali imetoa maelekezo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya na mikoa kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2010/11 na kutoa majibu ya hoja zote kabla ya Desemba, mwaka huu.

Alisema lengo ni kuhakikisha kwamba katika Mkutano wa Bunge la Februari, serikali inakuwa na majibu yote ili kuyatoa bungeni kwenye Mkutano wa Bunge wa Aprili.

“Tumetoa miezi mitatu kuanzia Mei wapitie na kujibu hoja zote za CAG kisha wazipeleke mkoani kama mkoa hautaridhika wazirudishe tena hadi tupate majibu sahihi. Tunataka itakapofika Januari serikali iwe imeshapata majibu ya uhakika,” alisema Pinda.

Pinda alisema: “Nimewaambia wenzangu wa Tamisemi tusiendelee na hii hoja ya onyo, hatutafika mbali. Anayekutwa na kosa msimamisheni na apelekwe mahakamani akapambane na sheria.”

WAKURUGENZI WAWILI MATATANI

Kutokana na msimamo huo, Pinda, alisema ametoa maagizo ya kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi wa Halmashauri za Sengerema na Misungwi na kisha wafikishwe mahakamani kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.

Aliwataka pia madiwani kuwa makini wanapopitia hesabu za halmashauri pamoja na ripoti ya CAG ili kuongeza utendaji na uwajibikaji kuanzia ngazi ya chini.

Alisema maelekezo hayo yametolewa pia kwa wizara zote pamoja na mashirika ya umma kuhakikisha yanajibu hoja za CAG na kuziwasilisha kwenye wizara za kisekta kwa ajili ya kujiridhisha.

AMSHUSHUA KIMORO

Akizungumzia Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimoro, ambaye hivi karibuni alitangaza kujiuzulu wadhifa huo, Pinda alisema ameshangaa kusikia hivyo kwa kuwa alikuwa kwenye orodha ya wale waliokuwa wameachwa.

“Rais alisema tusitangaze bila kuwaarifu watakaoachwa. Alijua ataondolewa. Sasa tunashangaa kwa nini alienda kujitangaza…huyu angekuwa tu mkweli,” alisema Pinda na kusababisha kicheko katika mkutano huo.

Bila kufafanua kwa undani, alisema pindi inapotokea mteule wa Rais anaachwa kwenye uteuzi mwingine kama siyo kwa sababu za umri ama maradhi, hizo sababu zingine zinakuwa nzito.

Hata hivyo, Kimoro alipokuwa akitangaza kujiuzulu wadhifa huo alidai kuwa ni kwa sababu serikali imeshindwa kuwawajibisha watendaji ambao siyo waaminifu, serikali kuruhusu kampuni za kununua kahawa mbichi, biashara ya vocha za ruzuku na sababu binafsi.

WAPYA WALIOTEULIWA

Miongoni mwa wakuu wa wilaya walioteuliwa na vituo vyao vya kazi kwenye mabano ni Novatus Makunga wa ITV/Radio One –Arusha (Hai); Jacqueline Liana wa gazeti la Uhuru (Magu); Muhingo Rweyemamu wa gazeti la Jamhuri (Handeni); Selemani Mzee Selemani wa Shirika la Utangazaji la Taifa –TBC (Kwimba) na Ahmed Kipozi wa TBC (Bagamoyo).

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum, Rosemary Kirigini (Meatu), Mboni Mgasa (Mkinga), Hanifa Selungu (Sikonge), Christine Mndeme (Hanang), Shaibu Ndemanga (Mwanga) na  Chrispin Meela (Rungwe).

Pia wamo Dk. Nasoro Hamidi (Lindi), Farida Mgomi (Masasi), Jeremba Munasa (Arumeru), Majid Mwanga (Lushoto), Mrisho Gambo ambaye alikuwa ni miongoni mwa makada wa Umoja wa Vijana wa CCM aliyekuwa amepewa karipio hivi karibuni  (Korogwe), Elias Tarimo (Kilosa), Alfred Msovella (Kiteto), Dk. Leticia Warioba (Iringa) na Dk. Michael Kadeghe (Mbozi).

Wengine ni Karen Yunus (Sengerema), Hassan Masala (Kilombero), Bituni Msangi (Nzega), Ephraem Mmbaga (Liwale), Antony Mtaka (Mvomero), Herman Kapufi (Same), Magareth Malenga (Kyela), Chande Nalicho (Tunduru), Fatuma Toufiq (Manyoni) na Seleman Liwowa (Kilindi).

Aliwataja wengine kuwa ni Josephine Matiro (Makete), Gerald Guninita (Kilolo), Senyi Ngaga (Mbinga), Mary Tesha (Ukerewe), Rodrick Mpogolo (Chato), Christopher Magala (Newala), Paza Mwamlima (Mpanda), Richard Mbeho (Biharamulo), Joshua Merumbe (Bunda), Constantine Kanyasu (Ngara), Yahya Nawanda (Iramba), Ulega Abdallah (Kilwa), Paul Mzindakaya (Busega) na Festo Kiswaga (Nanyumbu).

Wengine katika orodha hiyo ni Wilman Ndile (Mtwara), Joseph Mkirikiti (Songea), Ponsiano Nyami (Tandahimba), Elibariki Kingu (Kisarawe), Suleiman Kumchaya (Tabora), Dk. Charles Mlingwa (Siha), Manju Msambya (Ikungi), Omar Kwaangw’(Kondoa), Venance Mwamoto (Kibondo), Benson Mpesya (Kahama), Daudi Ntibenda (Karatu), Ramadhani Maneno (Kigoma), Sauda Mtondoo (Rufiji), Gulamhusein Kifu (Mbarali) na Esterina Kilasi (Wanging’ombe).

Wengine katika orodha ya wateule wapya ni Subira Mgalu (Muheza), Martha Umbula (Kongwa), Agnes Hokororo (Ruangwa), Regina Chonjo (Nachingwea), Wilson Nkhambaku (Kishapu), Amani Mwenegoha (Bukombe), Hafsa Mtasiwa (Pangani), Rosemary Senyamule (Ileje), Luteni Kanali Ngemela Lubinga (Mlele), Iddi Kimanta (Nkasi) na Lucy Mayenga (Uyui).

WA ZAMAMI WALIOPONA

Katika orodha ya waliopona, Waziri Mkuu, alisema baadhi wameteuliwa na kubaki kwenye wilaya walizokuwa wanaziongoza na wengine wamehamishwa.

Aliwataja waliobaki kuwa ni James Ole Millya (Longido), Mathew Sedoyeka (Sumbawanga), Fatuma Kimario (Igunga), Kapteni mstaafu James Yamungu (Serengeti), Luteni mtaafu Abdallah Kihato (Maswa), Sarah Dumba (Njombe), Jowika Kasunga (Monduli), Elizabeth Mkwasa (Bahi) na Kanali Issa Njiku (Misenyi).

Wengine ni John Henjewele (Tarime), Elias Lali (Ngorongoro), Raymond Mushi (Ilala), Francis Miti (Ulanga), Evarista Kalalu (Mufindi), Mariam Lugaira (Misungwi), Anna Magowa (Urambo), Anatory Choya (Mbulu), Fatma Ali (Chamwino), Deodatus Kinawiro (Chunya), Ibrahim Marwa (Nyang’wale) na Dk. Norman Sigala (Mbeya).

Katika orodha hiyo aliwataja pia Moshi Chang’a (Mkalama), Jordan Rugimbana (Kinondoni), Georgina Bundala (Itilima), Halima Kihemba (Kibaha), Manzie Mangochie (Geita), Abdula Lutavi (Namtumbo), Zipporah Pangani (Bukoba), Dk. Ibrahim Msengi (Moshi), Kanali Cosmas Kayombo (Kakonko), Lembris Kipuyo (Muleba), Elinasi Pallangyo (Rombo), Queen Mlozi (Singida), Juma Madaha (Ludewa), Angelina Mabula (Butihama), Hadija Nyembo (Uvinza) na Ernest Kahindi (Nyasa).

Wengine ni Peter Kiroya (Simanjiro), John Mongella (Arusha), Baraka Konisaga (Nyamagana), Husna Mwilima (Mbogwe), Sophia Mjema (Temeke), Francis Isaac (Chemba), Abihudi Saidea (Momba), Khalid Mandia (Babati) na Anarose Nyamubi (Shinyanga).

Kadhalika wamo Dani Makanga (Kasulu), Amina Masenza (Ilemela), Mercy Silla (Mkuranga), Christopher Kangoye (Mpwapwa), Luteni Edward Lenga (Kalambo), Halima Dendego (Tanga), Lephy Gembe (Dodoma), Said Amanzi (Morogro), Jackson Msome (Musoma) na Elias Goroi (Rorya).

Aliwataja Luteni Kanali Benedict Kitenga (Kyerwa), Erasto Sima (Bariadi), Nurdin Babu (Mafia), Khanifa Karamagi (Gairo), Gishuli Charles (Buhigwe), Saveli Maketta (Kaliua) na Darry Rwegasira (Karagwe).

CHANZO: NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni

No comments:

Post a Comment